Create successful ePaper yourself
Turn your PDF publications into a flip-book with our unique Google optimized e-Paper software.
SMART CLASS
BUKUA KIDIJITALI, FURSA KWA WALIMU
MEMA TEAM
Ulishawahi kufikiria itafikia kipindi watu watachagua
kubaki nyumbani na kusoma kupitia mifumo ya
kimtandao badala ya kwenda shuleni? Janga la
COVID19 lilitupa funzo juu ya uwezekano wa jambo
hili.Wakati wa COVID19, mwezi March 2020 shule
zilifungwa na tulishuhudia vituo kadhaa vya Tv na
majukwaa ya kidijitali yakitoa elimu kwa wanafunzi.
Moja ya majukwaa hayo ni Smart Class ambao
wanatoa huduma ya mafunzo kwa wanafunzi wa shule
za msingi na sekondari kwa njia ya mtandao na nje ya
mtandao. Adam Duma, ni moja ya waanzilishi wenza
wa Smart Class na hapa anatuelezea kuhusu ubunifu
huu.
Mlipata wapi mtaji?
UBUNIFU
Unapoanzisha wazo lazima uangalie nani anaweza
kuwekeza pesa zake. Hili wazo lilikuja mimi bado
nipo chuo mwaka wa pili, kuna mwalimu wa Chuo
Kikuu cha Dar Es Salaam nilimshirikisha na akawa
tayari kuwekeza baadhi ya pesa kutoka kwenye
mshahara wake kama mtaji. Mimi niliomba msaada
wa kifedha kutoka nyumbani na pia yule mwalimu
alikuwa na rafiki yake anafanya kazi Nokia na yeye
aliungana nasi na hatimaye tukaanzisha kampuni.
Siku zilivyozidi kusonga tukaanza kupokea pesa
kutoka kwa wafadhili tofauti.
Smart Class ni nini?
Ni jukwaa la mtandaoni linalokutanisha walimu, wazazi
na wanafunzi na inapatikana nchini Tanzania na
Kenya kwa njia ya tovuti kutoa mafunzo ya ziada
maarufu ‘tuition’. Makundi yote haya matatu yanajisajili
bure na kisha kuanza kutumia huduma hii. Smart Class
inamuunganisha mwanafunzi au mzazi ambao ndio
wasimamizi wa taaluma kwa watoto wao na kisha
anachagua aidha asome ‘online’ au mwalimu amfuate
nyumbani. Mafunzo yanapokamilika, mwanafunzi
anatupatia ripoti ya huduma aliyopewa na malipo
yanafanyika Smart Class kisha mwalimu hupokea 85%
na 15% hubakia kwetu. Gharama za mafunzo
zinatofautiana kulingana na muda na mfumo wa
utolewaji wake, kwa ‘online’ ni nafuu kuliko kufuatwa
nyumbani ‘offline’.
Wazo liliibuka vipi?
Wazo tulianza nalo mwaka 2018 pamoja na wenzangu
wawili wakati huo tulikuwa Chuo Kikuu
cha Dar Es Salaam. Tulifanya utafiti kwa takribani
mwaka mmoja ili kubaini ni namna gani tutaweza
kutatua tatizo la ajira kwa walimu wakati wakisubiri ajira
za kudumu kutoka serikalini na kuondoa pengo la elimu
bora. Baada ya kufanya utafiti tulishiriki katika
maonyesho ya Research Innovation Week 2019
yanayoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na
mapokeo tuliyoyapata ndio yalitushawishi njia pekee ya
kutatua changamoto hii ni teknolojia na wazo la Smart
Class tukaanza kulifanyia kazi na kuizindua rasmi
mwaka huo huo.
Mapokeo kwa waTanzania yakoje?
Mapokeo ni mazuri kwa maana ya idadi ya
watumiaji tulio nao ambao kwa Tanzania wanafika
12,000 (walimu, wazazi na wanafunzi). Shule
zilipofungwa kipindi cha COVID19 naweza kusema
kwetu ilikuwa ni neema kwa sababu kulikuwa na
ongezeko kubwa la watumiaji wa jukwaa letu.
Changomoto iliyopo kwa Tanzania kunapoibuka
teknolojia mpya watu wengi huwa wanakuwa
wagumu kuipokea kwa haraka. Ila taratibu watu
wanazidi kuelea huduma tunayotoa.
Mliwezaje kufika Kenya?
Kwanza tulifikiria kujitanua Kenya kutokana na
uelewa mkubwa uliopo kule katika masuala ya
teknolojia. Kuna watumiaji wengi wa intaneti,
kwenda kule ilikuwa ni kulifikia kwa urahisi soko
ambalo tayari lipo. Kuna jamaa yetu anaitwa
Kimathi aliacha kazi na kusimamia mchakato
mzima wa kuanzisha Smart Class Kenya na ndio
msimamizi pamoja na watu wengine watatu.
Kenya tunawatumiaji zaidi ya 5,000 wa Smart
Class.
Mnajionaje miaka 5 ijayo?
Kuwa jukwaa kubwa la elimu Afrika. Kwa
mwalimu, mzazi au mwanafunzi anaweza kuipata
Smart Class kwa kutembelea
www.smartclasstz.com na kuanza kutumia
huduma zetu.
27 | AUG 2021 MEMA MAGAZINE